Iran yaitaka serikali ya Ufaransa iache kukandamiza raia wanaoandamana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58832-iran_yaitaka_serikali_ya_ufaransa_iache_kukandamiza_raia_wanaoandamana
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo imeitaka serikali na polisi wa Ufaransa waache kukandamiza waandamanaji nchini humo.
(last modified 2026-09-02T10:39:46+00:00 )
Jan 30, 2020 03:39 UTC
  • Iran yaitaka serikali ya Ufaransa iache kukandamiza raia wanaoandamana

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo imeitaka serikali na polisi wa Ufaransa waache kukandamiza waandamanaji nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesambaza mkanda wa video unaoonesha jinsi jeshi la polisi la Ufaransa linavyowakandamiza waandamanaji  na kusema kuwa, maandamano ya wananchi hao ni ya haki, hivyo polisi na serikali ya Ufaransa wanapaswa kuacha mara moja kukandamiza raia.

Tangu tarehe 17 Novemba 2018 hadi hivi sasa Ufaransa imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi wanaopinga siasa mbovu na kandamizi za serikali ya nchi hiyo.

Afisa wa polisi wa Ufaransa akimpiga kirungu raia muandamanaji

 

Hata hivyo maandamano hayo mara zote yamekuwa yakikandamizwa na jeshi la polisi linalotumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na raia hao.

Hadi hivi sasa watu 11 wameshauawa na karibu 14 elfu wengine wameshajeruhiwa na kutiwa mbaroni na polisi wa Ufaransa.

Cheche ya maandamano hayo maarufu kwa jina la "Maandamano ya Vizibao vya Njano" ilitokana na siasa za kiuchumi za rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron hususan za kuongezea ushuru mafuta. Hata hivyo maandamano hayo yaligeuka haraka na kuwa ya kisiasa ya kulalamikia mfumo mzima wa kibepari wa nchi za Magharibi.

Kuanzia wakati huo hadi hivi sasa, siku zote Ufaransa inashuhudia migomo na maandamano. Mwezi Disemba 2019, maelfu ya walimu na wafanyakazi walifanya mgomo mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika miongo ya hivi karibuni nchini humo, kulalamikia siasa za Macron za marekebisho ya muda wa kustaafu.