Iran yasema iko tayari kwa mazungumzo lakini haikubali kushinikizwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59101-iran_yasema_iko_tayari_kwa_mazungumzo_lakini_haikubali_kushinikizwa
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haijafunga mlango wa kufanya mazungumzo kuhusu mradi wake wa nyuklia lakini katu haiwezi kukubali kuburuzwa na kuwekwa chini ya mashinikizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2020 04:05 UTC
  • Iran yasema iko tayari kwa mazungumzo lakini haikubali kushinikizwa

Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haijafunga mlango wa kufanya mazungumzo kuhusu mradi wake wa nyuklia lakini katu haiwezi kukubali kuburuzwa na kuwekwa chini ya mashinikizo.

Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomikili la Iran aliyasema hayo jana Jumanne mjini Vienna katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, na kuongeza kuwa "uhusiano wa Iran na IAEA ni mzuri na umejengeka katika misingi ya maelewano; na kama taasisi ya kimataifa, wakala huu haupaswi kushinikizwa na kuburuzwa kisiasa katika kufanya maamuzi yake."

Salehi ameeleza bayana kuwa, taifa hili linakaribisha mazungumzo yenye mantiki lakini kamwe haliwezi kuchukua hatua yoyote kutokana na mashinikizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, ameipongeza Iran kwa ushirikiano wake katika nyuga mbali mbali na kuitaka iendelee kuwa na uhusiano amilifu na IAEA kama ilivyokuwa huko nyuma.

Mradi wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani

Baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 8 mwaka 2018, nchi za Ulaya hususan Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ziliahidi kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran katika mapatano hayo.

Hata hivyo licha ya kutoa matamshi ya kupinga maamuzi ya Marekani kuhusu JCPOA, lakini nchi hizo za Ulaya hazijachukua hatua za kivitendo kutekeleza ahadi zao za kulinda mapatano hayo, jambo ambalo liliilazimisha Iran kupunguza uwajibikaji wake hatua kwa hatua kwenye mapatano hayo ya kimataifa.