Uchaguzi umemalizika, zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Iran
Ijumaa ya jana tarehe 21 Februari mamilioni ya Wairani walielekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa kwanza mdogo wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran.
Kufanyika mara kwa mara chaguzi hapa nchini na kurejea kwenye kura za wananchi katika masuala mbalimbali ni miongoni mwa fahari za utawala wa Kiislamu hapa nchini. Uchaguzi katika Jamhuri ya kiislamu ya Iran, ni kielelezo cha kushirikishwa wananchi katika kuchukua maamuzi muhimu ya kisiasa na kijamii na zoezi hilo linatambuliwa kuwa ni wajibu wa kisheria na kidini na haki ya kiraia ya kila Muirani. Kwa sababu hiyo pia utawala wa Kiislamu hapa nchini uliasisiwa kwa kutegemea kura za wananchi, na suala la kuainisha mambo muhimu kwa kurejea kwenye kura za wananchi linatambuliwa na katiba ya nchi kuwa msingi wa demokrasia ya kidini ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Katika uchaguzi wa jana raia milioni 57, laki 9, na 18 elfu na 159 wa Iran walikamilisha masharti ya kupiga kura na zaidi ya wagombea elfu saba na 157 wanachuana katika majimbo 208 ya uchaguzi kwa ajili ya viti 290 vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu. Baada tu ya kumalizika uchaguzi huo jana usiku ambao muda wake ulirefushwa kwa masaa kadhaa kutokana na idadi kubwa ya watu, zoezi la kuhesabu kura lilianza na bado linaendelea katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi. Tangu miezi kadhaa iliyopita zimefanyika zitihada kubwa za kuhakikisha kwamba, uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa sheria, maadili ya kisiasa na haki za kijamii zinazodhamini usalama na afya ya uchaguzi huo.
Uchaguzi, kwa kawaida, huwa na taathira zake za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kwa msingi huo maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamefanya njama za aina mbalimbali kuwavunja moyo wananchi na kujaribu kuwashawishi wasishiriki katika zoezi hilo. Harakati kama hizi za maadui si jambo jipya kwa taifa la Iran. Kutokana na uzoefu wao wa miaka iliyopita Wairani wanajua vyema kwamba, njama hizo za maadui zinafuatilia malengo kadhaa, muhimu zaidi likiwa ni kutaka kudhoofisha moyo wa wananchi na kuwaondoa katika medani muhimu ya kushiriki katika masuala ya kisiasa ya nchi yao. Hata hivyo njama hizo za maadui zimekuwa zikigonga mwamba mwaka baada ya mwingine.
Ukweli huu umeakisiwa katika hotuba ya siku chache zilizopita ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei pale aliposema kwamba: Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita Wamarekani wametumia zilaha zote za kisiasa, kiusalama, kiuchumi, kiutamaduni, vyombo vya habari na kila walichoweza kwa ajili ya kuuondoa madarakani utawala wa Kiislamu nchini Iran lakini Jamhuri ya Kiislamu si tu kwamba haijaanguka, bali pia imeimarika zaidi mara elfu moja na Marekani imedhoofika zaidi.
Wananchi wa Iran daima wamekuwa wakikwamisha njama mbalimbali za maadui wa taifa lao kwa kuhudhuria kwa wakati mwafaka na katika vipindi nyeti na vigumu katika medani mbalimbali licha ya mashaka na baadhi ya machungu wanayokabiliana nayo. Kuchaguliwa kwa wabunge wanaofaa kunaweza kuimarisha mhimili huo muhimu wa dola na kujenga Bunge imara zaidi linaloweza kusaidia jitihada za kuboresha maisha ya wananchi na kutunga sheria za jinsi ya kukabiliana ipasavyo na changamoto mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Kwa kutilia maanani uhakika huo, hapana shaka kuwa kura ya kila mwananchi ina umuhimu mkubwa katika kuainisha mustakbali wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yao. Vilevile uchaguzi huo unawapa wananchi fursa ya kutathmini upya utendaji wa wawakilishi wao, kurekebisha pale walipoenda mrama na kutia nguvu na kasi zaidi maendeleo na mafanikio yaliyopatikana.
Kwa sasa inatupasa kusubiri na kuona matokeo ya uchaguzi na kura za wananchi wa Iran ili tuweze kujua muundo wa Bunge lijalo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.