Iran yaonya kuhusu bidaa zisizo na msingi katika wakala wa IAEA
Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika asasi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria amejibu ripoti mpya ya wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusema kuwa, Tehran imo mbioni kuzuia uanzishwaji wa bidaa zisizo na msingi na hatari katika wakala huo.
Jumanne ya jana Wakala wa Kimatiafa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ulitangaza katika ripoti yake mpya kwamba, eti Iran haijaruhusu kutembelewa maeneo yake matatu kama ambavyo pia eti haijatoa ushirikiano unaotakiwa kuhusiana na majibu ya maswali ya wakala huo kuhusiana na mada za nyuklia ambazo hazikutangazwa hapo kabla.
Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika asasi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria akizungumza na vyombo vya habari leo amesema kuwa, inasikitisha kuwa, kwa mara nyingine tena Marekani na utawala haramu wa Israel zinafanya njama za kuvuruga uhusiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Ameeleza kuwa, Marekani na utawala haramu wa Israel zinaushinikiza Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ili uache kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni zake.
Aidha Kazem Gharib Abadi, amebainisha kwamba, kama mataifa ya dunia hayatachukua hatua za kimsingi na madhubuti kwa ajili ya kukabiliana na njama pamoja na uzushi wa mashirika ya kijasusi, basi mamlaka yao ya kujitawala yatatiwa doa na kuchafuliwa.