Mar 26, 2020 11:08 UTC
  • Waziri Zarif: Pompeo ni Waziri wa Chuki wa Marekani

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali mienendo ya mwenzake wa Marekani, Mike Pompeo ya kueneza chuki, uhasama na propaganda dhidi ya Iran na kumtaja waziri huyo wa utawala wa Donald Trump kama Waziri wa Chuki.

Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Muhammad Javad Zarif amesema: Hata katika kipindi cha janga la kimataifa, Pompeo haachi kueneza propaganda za daraja ya tatu. Unashangaa iwapo ni Waziri wa Mambo ya Nje au Waziri wa Chuki.

Dakta Zarif amesema licha ya Pompeo kukosolewa vikali, lakini ameendelea kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran, kuchochea vita, kuendeleza ugaidi wa kiuchumi, kuua wasio na hatia, na kukwamisha jitihada za kimataifa za kukabiliana na ugonjwa wa covid-19.

Kauli ya Dakta Zarif ni radiamali kwa matamshi ya kijuba ya Pompeo, aliyedai hivi karibuni kuwa Rais Hassan Rouhani wa Iran anaendesha visivyo mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari unaosababishwa na kirusi cha corona hapa nchini.

Jitihada za kupambana na corona nchini Iran licha ya vikwazo vya kidhalimu vya US

Licha ya kuibuka virusi angamizi vya corona ulimwenguni ikiwemo Iran, lakini Washington imeshupalia sera za vikwazo vya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran na imekuwa ikitangaza mtawalia vikwazo vipya dhidi ya Tehran.

Mwenendo huu usio wa kibinadamu wa Marekani umeendelea kukosolewa na mataifa mbalimbali ya dunia ambayo sasa yanaitaka Washington ikomeshe siasa zake hizo zisizo za kiutu.

Tags