Iran yakanusha madai ya kujiri mlipuko katika kituo cha nyuklia
Shirika la Iran la Nishati ya Atomiki limekanusha madai ya kujiri mlipuko katika kituo cha nyuklia cha Shahidi Rezaei-Nejad kati kati mwa Iran.
Idara ya Habari ya Shirika la Iran la Nishati ya Atomiki ilitoa taarifa Jumanne kufuatia madai ya wapinzani wa Mapinduzi ya Kiislamu katika vyombo vya habari ajinabi kuwa eti kumejiri mlipuko katika Kituo cha Nyuklia cha Shahidi Rezaei-Nejad katika mkoa wa Yazd kati kati mwa Iran.
Taarifa hiyo imesema hakuna mlipuko wowote uliojiri katika taasisi hiyo ya nyuklia na kwamba wanaopinga Mapinduzi ya Kiislamu wanaoishi nje ya Iran wametoa taarifa hizo katika fremu ya kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni utawala wa kigaidi na unaopenda vita.

Aidha taarifa hiyo imesema madai hayo yasiyo na msingi yametolewa kwa lengo la kuibua hali ya kukosa matumaini na yanaenda sambamba na mashinikizo ya hali ya juu kabisa dhidi ya taifa la Iran.
Shirika la Iran la Nishati ya Atomiki pia limetangaza kuwa picha za satalaiti zilizosambazwa hazihusiani na Kituo cha Nyuklia cha Shahidi Rezaei-Nejad.
Kituo hicho cha nyuklia kina kiwanda cha kuzalisha keki ya njano, ambayo ni mada ya madini ya urani inayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia. Kituo cha Nyuklia cha Shahidi Rezaei-Nejad, ambacho kinasimamiwa kikamilifu na wataalamu Wairani, kina uwezo wa kuzalisha tani 60 kwa mwaka za keki hiyo ya njano na kilianza rasmi kazi zake mwaka 2013.