Jul 17, 2020 08:05 UTC
  • Zarif: Iran haitalipa taifa lolote hata shibri moja ya ardhi yake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria juu ya makubaliano ya miaka 25 ya ushirikiano kati ya Iran na China na kusisitiza kuwa, katu Jamhuri ya Kiislamu haitapeana hata shibri moja ya ardhi yake au kuipa nchi yoyote ile ikiwemo China, haki maalumu ya kutumia maeneo yake.

Katika ujumbe wake kupitia Twitter Alkhamisi ya jana, Muhammad Javad Zarif kwa mara nyingine tena amekanusha vikali madai kuwa Iran imeiuzia China kisiwa chake cha Kish katika Ghuba ya Uajemi. 

Dakta Zarif amesema, "taarifa hizi si za kweli, na wala hazina hata chembe ya ukweli ndani yake. Hatujapeana hata mita moja ya ardhi yetu au kuipa nchi yoyote ile ikiwemo China, haki maalumu ya kutumia maeneo ambayo yako ndani ya mamlaka yetu."

Siku chache zilizopita pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitoa maelezo ya kina kuhusu rasimu ya mapatano ya ushirikiano wa miaka 25 baina ya Iran na China na kusema kuwa, uhusiano wa nchi hizo mbili umejengeka katika msingi wa maslahi ya pamoja na kuheshimiana.

Zarif amesema mchakato wa kutayarisha mapatano hayo ulianza wakati Rais Xi Jinping wa China alipoitembelea Iran mwaka 2016, ambapo nchi mbili zilisisitizia ulazima wa kuwepo mtazamo wa muda mrefu wa uhusiano wao, na kwamba utayarishaji wa mapatano hayo ungali unaendelea.

Rais Xi Jinping wa China alipoitembelea Iran mwaka 2016 na kukutana na Rais Hassan Rouhani

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China zinafanya jitihada za kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili kieneo na kimataifa kwa mujibu wa mpango huo wa ushirikiano wa miaka 25.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Post la Marekani ni kuwa: Mpango kamili wa ushirikiano wa miaka 25 kati ya Iran na China ambao ni mpango wa ushirikiano wa kistratejia, mbali na kuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa Tehran, vilevile ni pigo kubwa kwa juhudi zilizofeli za serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran. 

Tags