Araqchi akanusha madai ya kuwepo ofisi ya Taliban nchini Iran
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amekabidhisha vikali madai ya kipropaganda kuwa kundi la wapiganaji wa Taliban la Afghanistan lina ofisi hapa nchini. Sayyid Abbas Araqchi aidha amekanusha vikali uvumi wa uwepo wa kundi la Taliban hapa nchini Iran, kwa jina la "Baraza la Mashhad."
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Tolo News la Afghanistan ambapo amekumbusha kuwa, "Marekani inayodai kuwa ni muitifaki wa Afghanistan imekuwa ikifanya mazungumzo na Taliban kuhusu mustakabali wa Waafghani, bila kuishirikisha serikali ya Kabul."
Sayyid Araqchi amesema kila mmoja anatambua ni nani aliyeliunda kundi la Taliban, kulifadhili na kufanya mazungumzo nalo. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesisitiza kuwa, Iran haina uhusiano wa aina hiyo na kundi la Taliban.
Kadhalika Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amepuuzilia mbali madai kuwa Iran imekuwa ikiwapa silaha wapiganaji wa kundi la Taliban huku akisisitiza kuwa, baadhi ya madola yanafanya juu chini kuharibu uhusiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Kabul.
Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilikadhibisha madai yaliyotolewa na gazeti la New York Times kwamba Moscow imeshirikiana na wapiganaji wa kundi la Taliban kuwaua wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan.
Marekani inaeneza habari hizi za kipropaganda katika hali ambayo, mapema mwezi uliopita, Mullah Baradar, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi la Taliban alionana na kufanya mazungumzo mjini Doha Qatar na Zalmay Khalilzad, mwakilishi maalumu wa Marekani na Jenerali Austin Scott Miller, kamanda wa wanajeshi wa Marekani na NATO nchini Afghanistan.