Iran: Hakuna anayejali tena urongo wa vyombo vya intelijensia vya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63448-iran_hakuna_anayejali_tena_urongo_wa_vyombo_vya_intelijensia_vya_marekani
Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afrika Kusini umetangaza kuwa, dunia bado haijasahu uongo wa vyombo vya intelijensia vya Marekani uliotumiwa kuanzisha vita dhidi ya Iraq.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 15, 2020 22:09 UTC
  • Iran: Hakuna anayejali tena urongo wa vyombo vya intelijensia vya Marekani

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afrika Kusini umetangaza kuwa, dunia bado haijasahu uongo wa vyombo vya intelijensia vya Marekani uliotumiwa kuanzisha vita dhidi ya Iraq.

Katika maelezo uliyoweka kwenye ukurasa wake wa Twitter chini ya mkanda wa filamu unaomuonyesha waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo akikiri kuwa vyombo vya intelijensia vya nchi hiyo vinasema uongo na kufanya udanganyifu, ubalozi wa Iran nchini Afrika Kusini umesema: Sera hizo zilizochakaa hazina soko tena, na hasa kutokana na kwamba, leo hii kinara wa diplomasia za rais Donald Trump wa Marekani ni mmoja wa waongo hao, ambaye kwa kweli ndiye mrongo mkuu.

Katika mkanda huo wa filamu, Pompeo anasikika akisema: "Mimi nilikuwa mkuu wa CIA (Shirika la Ujasusi la Marekani). Tulisema uongo, tulifanya udanganyifu na tuliiba..."

Mike Pompeo

Hivi majuzi, jarida la POLITICO la nchini Marekani lilinukuu ripoti za intelijensia za Washington pamoja na maafisa wa karibu na serikali ya nchi hiyo wanaodai kwamba, Iran ina mpango wa kutaka kumuua balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Saeed Khatibzadeh amekanusha tuhuma hizo za kiuadui na zenye malengo maalumu na akawashauri viongozi wa Marekani waache kutumia mbinu hizo zilizopitwa na wakati kwa ajili ya propaganda dhidi ya Iran katika uga wa kimataifa.

Khatibzadeh amesema, katika wakati huu wa kukaribia kufanyika uchaguzi wa rais wa Marekani hatua za aina hiyo na uenezaji habari za uzushi kama hizo unaweza ukaendelea kushuhudiwa katika siku zijazo, lakini akasisitiza kwamba: Hapana shaka hatua hizo hazitakuwa na natija yoyote, zaidi ya kuongezwa kwenye orodha ndefu ya kufeli na kugonga mwamba mtawalia Marekani katika kukabiliana na Iran.../