Zarif amwambia Donald Trump: Ni wakati wa kuamka
-
Muhammad Javad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amenusha propaganda chafu zinazofanywa na vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu madai eti Iran inafanya mpango wa kumuua balozi Marekani nchini Afrika Kusini na kusema huu ni wakati wa kuamka.
Muhammad Javad Zarif amesema katika ujumbe wake wa mtandao wa Twitter kuhusu madai hayo kwamba: Uongo wa daima na tahadhari za uongo zimempotosha Donald Trump na kumfanya amuue kigaidi adui nambari moja wa kundi la Daesh.
Hivi majuzi, jarida la POLITICO la nchini Marekani lilinukuu kile kilichodaiwa ni ripoti za intelijensia za Washington pamoja na maafisa wa karibu na serikali ya nchi hiyo wanaodai kwamba, Iran ina mpango wa kutaka kumuua balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini.
Jarida hilo lilinukuu chombo kisichojulikana na kudai kuwa Tehran ilikuwa na mpango wa kumuua balozi Lana J. Marks wa Marekani mjini Pretoria kwa lengo la kulipiza kisasi cha mauaji yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Saeed Khatibzadeh amekanusha tuhuma hizo za kiuadui na zenye malengo maalumu na akawashauri viongozi wa Marekani waache kutumia mbinu hizo zilizopitwa na wakati kwa ajili ya propaganda dhidi ya Iran katika uga wa kimataifa.