Spika: Nchi za Kiislamu zisifuate nyayo za Marekani za kuiwekea vikwazo Iran
(last modified Tue, 20 Oct 2020 07:40:35 GMT )
Oct 20, 2020 07:40 UTC
  • Spika: Nchi za Kiislamu zisifuate nyayo za Marekani za kuiwekea vikwazo Iran

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka serikali za nchi za Kiislamu zisikubali kufuata nyayo za Marekani za kuiwekea vikwazo Iran katika kipindi hiki cha janga la corona.

Muhammad Baqer Qalibaf amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Azhar Azizan Harun, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Malaysia na kuongeza kuwa, "katika hali ya sasa ambapo kila mmoja anakabiliana na mgogoro wa janga la corona, utawala wa Marekani umeliwekea taifa la Iran vikwazo vya kikatili na vilivyo kinyume na sheria. Tunataraji nchi rafiki na za Kiislamu hazitafuata mkumbo huo."

Sanjari na kuashiria juu ya umuhimu wa kuimarisha umoja miongoni mwa nchi za Kiislamu, Qalibaf amebainisha kuwa, Iran na Malaysia kama nchi mbili muhimu za ulimwengu wa Kiislamu, zinapaswa kuboresha umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu na kujiepusha na migawanyiko.

Umoja wa Umma

Kwa upande wake, Azhar Azizan Harun, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Malaysia amegusia kunako vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, "Malaysia inashikilia msimamo wake juu ya vikwazo hivyo, hatutambui vikwazo haramu na ambavyo haviendani na maazimio ya Umoja wa Mataifa."

Amesema Tehran na Kuala Lumpur zitaendelea kushirikiana katika jitihada za kuziunganisha nchi za Kiislamu ili kwa pamoja ziweze kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayozikabili. 

Tags