Meja Jenerali Salami: Maadui wangojee jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema: Maadui wangojee huku wakijua lazima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua kujibu kitendo cha kigaidi cha kumuua mwanasayansi wake bingwa wa masuala ya nyuklia na ulinzi.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo pembeni ya hafla iliyofanyika jana Jumanne katika makao makuu ya jeshi hilo hapa mjini Tehran kumuenzi mwanasayansi shahidi Mohsen Fakhrizadeh; na akaongeza kwamba: Maadui walioikamia Iran ya Kiislamu inawapasa wajue kuwa kifo cha ushahidi ni taa inayomurika njia; na njia inayofunguliwa na mashahidi katu haitafungika milele.
Meja Jenerali Salami amebainisha kuwa: Kila nukta anayoilenga na kuiandama adui inamaanisha kuwa ni nukta chanya na ya mafanikio kwa Iran na yenye kuwatia hofu maadui; na kuchukua hatua za kijinai kama kufanya mauaji ya kigaidi kunamaanisha kwamba kuna ulazima wa kuendelea kulea na kuandaa watu walio mfano wa shahidi Fakhrizadeh.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa njia ya shahidi Fakhrizadeh itaendelezwa na wanafunzi wake kwa azma na irada kubwa zaidi na akaeleza kwamba, mauaji ya kigaidi na hatua zingine ovu zinazochukuliwa na maadui hazitakuwa na matunda mengine kwao isipokuwa kuyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yasonge mbele kwa kasi zaidi.
Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa masuala ya nyuklia na ulinzi wa Iran aliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika eneo la Absard, Damand hapa mjini Tehran siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba.
Mauaji hayo ya kigaidi ya shahidi huyo mwenye hadhi ya juu yaliyofanywa na magaidi waoga na wenye nyoyo zilizopofuka yamelaaniwa kimataifa, ambapo hadi sasa nchi nyingi zikiwemo Syria, Russia, Uswisi, Venezuela, Afrika Kusini, Uturuki, Qatar, Kuwait, Lebanon, Jordan na Afghanistan zimelaani jinai hiyo.../