Jenerali Salami: Iran ina kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya kumshinda adui
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema taifa hili linamiliki kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya kutoa pigo kwa maadui na wavamizi.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo jana Alkhamisi katika kikao cha maadhimisho ya kutimia mwaka mmoja tokea auawe shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Amesema, "vyombo na zana tulizo nazo ni za aina yake, nawashauri maadui waweke pembeni ndoto zao za Alinacha, na wakae mbali na wananchi wa Iran."
Jenerali Salami amekariri kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa Jamhuri ya Kiislamu italipiza kisasi cha damu ya kamanda shahidi Qassim Soleimani kwa waliomuua.
Ameashiria kuhusu mauaji ya kigaidi ya mwanasayansi bingwa wa taifa hili, Shahidi Mohsen Fakhrizadeh na kubainisha kuwa, jinai za aina hiyo katu haziwezi kulemaza ustawi wa kisayansi wa taifa la Iran.
Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa masuala ya nyuklia na ulinzi wa Iran aliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika eneo la Absard, Damand hapa mjini Tehran tarehe 27 Novemba mwaka huu.