Rais Rouhani: Serikali inafuatilia kila lahadha ili kuvifanya vikwazo kutokuwa na taathira
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65417-rais_rouhani_serikali_inafuatilia_kila_lahadha_ili_kuvifanya_vikwazo_kutokuwa_na_taathira
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, serikali inafanya hima na juhudi kubwa tena kila lahadha kuhakikisha kwamba vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya taifa hili vinafubaa na kutokuwa na taathira.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 26, 2020 14:33 UTC
  • Rais Rouhani: Serikali inafuatilia kila lahadha ili kuvifanya vikwazo kutokuwa na taathira

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, serikali inafanya hima na juhudi kubwa tena kila lahadha kuhakikisha kwamba vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya taifa hili vinafubaa na kutokuwa na taathira.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika kikao cha Kamati ya Taifa ya Kupambana na Corona kilichofanyika hapa mjini Tehran ambapo ameashiria hatua za kijuba na ukwamishaji mambo za Marekani kwa ajili ya taifa hili kupata chanjo ya corona na kusema kuwa, serikali ya Washington imelikwamisha taifa hili katika juhudi zake za kununua chanjo ya Corona na vyombo vya habari vilivyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kila siku vimekuwa vikipata visingizo na hivyo kufuata mkumbo huo wa adui.

Dakta Hassan Rouhani amesisitiza kuwa, popote pale ambapo kutapatikana chanjo ya kuaminika ya corona na Wizara ya Afya na Mafunzo ya Utabibu ikatangaza na kuthibitisha kwamba, chanjo hiyo ni ya kuaminika, basi serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha chanjo hiyo inanunuliwa na kuletwa hapa nchini.

Mbali na kuagiza chanjo ya Covax, Iran ipo mbioni kujizalishia chanjo yake

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Gavana wa Benki Kuu ya Iran amesema nchi hii imefanikiwa kutuma katika akaunti ya benki ya Uswisi Yuro milioni 200 kwa ajili ya kununua chanjo ya ugonjwa wa Covid-19. 

Abdolnaser Hemmati amesema baada ya jitihada za siku 10, benki hiyo kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Iran imefanikiwa kutuma kwa mbinde fedha hizo kutokana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani, kwa ajili ya kununua dozi milioni 16.8 za chanjo ya Covax.