Dec 30, 2020 12:44 UTC
  • Majaribio ya chanjo ya kwanza ya COVID-19 iliyotengenezwa nchini Iran

Chanjo ya corona au COVID-19 iliyotegenezwa na watafiti Wairani imeanza kufanyiwa majaribio kwa wanadamu siku ya Jumanne 29 Disemba ambapo watu waliojitolea wamedungwa chanjo hiyo.

Daktari Saeed Namaki, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza kuhusu chanjo hiyo ya Iran kufanyiwa majaribio kwa mwanadamu na kusema: "Leo ni kati ya siku zenye matumaini zaidi kwa taifa la Iran. Kufuatia jitihada za wasomi na wataalamu wa Iran kuhusu COVID-19,  tumepita awamu ya utafiti na sasa tumeweza kumdunga mwandamu chanjo hii."

Chanjo hiyo ambayo inajulikana kama COVIRAN Barekat imetegenezwa katika Idara ya Utafiti ya Taasisi ya Utekelezaji wa Maagizo ya Imam Khomeini (MA)

Janga la COVID-19 ni janga la kimataifa. Ugumu wa kukabiliana na janga la corona Iran umebainika zaidi kutokana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya nchi hii.

Katika uga huo, Marekani imekuwa ikifanya juu chini kuhakikisha kuwa Iran haipati dawa na vifaa vya kitiba kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa corona. Hata baada ya Iran kutangaza kuwa tayari kununua chanjo ya homa kali ya influenza ambayo huenea zaidi wakati wa msimu huu wa baridi nchini, Marekani ilihakikisha kuwa imeweka vizingiti ili Iran isipate kununua chanjo hiyo.

Mwanadamu wa kwanza kujitolea kudungwa chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa Iran inayojulikana kama COVIRAN Barekat akidungwa chanjo hiyo katika sherehe iliyofanyika Tehran Disemba 29, 2020

Maadui wa taifa la Iran huwa wanatumia kila mbinu kulipa pigo taifa la Iran. Serikali nyingi duniani zimekabiliwa na mtihani mkubwa kuhusu namna ya kukabiliana na kirusi cha corona. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kuwa haiwezi kusalimu amri mbele ya matatizo na vikwazo vya maadui.

Katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata chanjo ya corona, Iran imekuwa ikifuatilia njia tatu. 

Njia ya kwanza ni kupitia kununua katika soko la kimataifa chanjo ambazo zimeainishwa katika mpango maalumu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya nchi zote za dunia. Hadi sasa chanjo za mashirika kadhaa zimeanza kutumiwa.  Chanjo ya  Oxford/AstraZeneca na Moderna ni chanjo ambazo zimeidhinishwa na WHO. Iran imeagiza dozi milioni 16 na laki nane  za chanjo hizo kwa ajili ya watu milioni nane na laki nne ambao wako katika makundi yenye hitajioo la kimsingi la chanjo. Kila mgonjwa hupata dozi mbili za chanjo hiyo.

Njia ya pili  ambayo Iran inatumia kupata chanjo ni kutegemea vyanzo vingine huru vya kimataifa na hadi sasa mazungumzo yanaendelea kuhusiana na hilo.

Njia ya tatu ambayo Iran imekuwa ikifuatilia katika kupata chanjo, ni ushirikiano  katika uzalishaji chanjo.

Kuhusiana na hilo, Iran inashirikiana kiteknolojia na moja ya mashirika ya kimataifa na imeingia katika uzalishaji wa chanjo katika  Taasisi ya Pasteur ya Iran.

Ikumbukwe kuwa Iran ina uzoefu wa karibu miaka 100 katika uzalishaji wa chanjo na imekuwa ikiuza chanjo zilizotegenezwa ndani ya nchi katika  maeneo mengine  duniani. 

Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki akizungumza katika sherehe za kuzindua majaribio ya chanjo ya COVID-19 iliyotegenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayojulikana kama COVIRAN Barekat

 

Katika kukabiliana na COVID-19, lengo kuu la wanasayansi na wasomi wa Iran limekuwa ni kuzalisha chanjo ndani ya nchi.  Kuhusiana na hilo, Iran imetumia uwezo wake wote wa kitaifa pamoja na irada imara katika kukabiliana na janga la COVID-19 na kulibadilisha tishio la janga hilo  kuwa fursa.  Hivi sasa jitihada za Iran zimezaa matunda na utengenezaji  wa chanjo ya corona ya Iran umefika katika kiwango cha majaribio kwa wanadamu na hatimaye kuzalishwa kwa wingi. Utegenezaji wa chanjo hiyo ya Iran unafanyikwa kwa uangalizi wa Shirika la Afya Duniani.

Inatazamiwa kuwa, kufuatia kuanza majaribio ya chanjo hiyo kwa mwanadamu, ifikapo mwaka mpya wa Kiirani wa 1400 Hijria Shamsia, ambao utaanza Machi 21, Iran itakuwa moja kati ya wazalishaji wakubwa wa chanjo ya COVID-19 katika eneo na hivyo itaweza kukidhi mahitaji yake katika uga huo.

Tags