Rouhani: Ulaya haijatekeleza ahadi zake; ikirejea katika majukumu yake nasi pia tutarejea
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran itarejea katika mapatano ya JCPOA kwa sharti kwamba Marekani na Ulaya nazo zitekeleze majukumu yao.
Akizungumza leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri, Rais Hassan Rouhani ameeleza kuwa, dunia nzima sasa imeungana na kuwa kitu kimoja ukitoa nchi chache tu, ikiitaka Marekani irejee katika majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA. Amesema kuwa iwapo itarejea katika majukumu yake Iran nayo itarejea haraka iwezekanavyo katika majukumu yake kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA.
Rais Rouhani ameashiria pia namna vita vya kiuchumi vya adui dhidi ya Iran vilivyogonga mwamba na kueleza kuwa: Hii leo nchi hii imekuwa na uhakika zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Amesema, vita vya kiuchumi vya adui vimefeli, na vimefikia katika siku zake za mwisho huku mabadilishano ya kibiashara ya washirika wa Iran katika eneo yakibadilika kikamilifu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amegusia kumbukumbu ya maadhimisho ya mwaka wa 42 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuashiria namna sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zilivyokuwa tofauti miaka iliyopita na kueleza kuwa: Mwaka huu wale wote ambao walikusudia kuyapigisha magoti mapinduzi haya miaka kadhaa iliyopita kupitia ugaidi na vita vyao vya kiuchumi hawapo tena.