Chanjo ya corona kuanza kutolewa wiki hii nchini Iran
-
Rais Rouhani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa chanjo ya corona itaanza kutolewa wiki hii hapa nchini kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa na Wizara ya Afya.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamisheni ya Taifa ya Kupambana na Corona. Ameashiria kwamba hivi sasa Iran inakaribia kukamilisha mwaka mzima tangu virusi vya corona viingie hapa nchini na kusema: Maambukizi ya virusi hivyo yameleta hali makhsusi kote duniani, kwa msingi huo njia bora zaidi ya kukabiliana navyo kuzuia maambukizi yake.
Amesisitiza kuwa hapa nchini zimefanyika juhudi za kutengeneza dawa zote maarufu na kuzisambaza mahospialini na kwamba iwapo pande zote zitashirikiana tunaweza kushinda maambukizi ya virusi vya corona.
Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa, asasi zote ziko tayari kwa ajili ya kutoa chanjo ya corona na kwa bahati nzuri shehena ya kwanza ya chanjo hiyo imeingia nchini; kwa msingi huo wiki hii na sambamba na sherehe za Wiki ya Alfajiri Kumi na maadhimisho ya kitaifa ya ushindi wa Mapnduzi ya Kiislamu hapa nchini, kutaanza kutolewa chanjo hiyo ya corona kwa mujibu wa vigezo vilivyoainishwa na Wizara ya Afya.
Amesema itafurahisha kutolewa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kwa sababu ndio wanaokabiliwa na hatari kubwa zaidi ya maambukizi ya corona na baada ya hapo chanjo itatolewa kwa watu wazima na wale wanosumbuliwa na magonjwa mengine.