Iran yakaribisha uundwaji wa serikali ya mpito Libya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekaribisha uundwaji wa serikali ya mpito nchini Libya.
Katika taarifa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Saeed Khatibzadeh amekaribisha matuko ya kikao cha pande husika za kisiasa Libya huko Geneva siku ya Ijumaa ambapo kulifikiwa mapatano ya kuundwa serikali ya mpito nchini Libya. Ameelezea matumaini yake kuwa serikali ya mpito ya Libya itaweza kuandaa mazingira yanayohitajika kwa ajili ya kufanyika uchaguzi.
Aidha amesema: "Nina matumaini kuwa serikali ya muda Libya itaweza kuleta uthabiti, utulivu na ustawi kwa ajili ya nchi hiyo kwa msingi wa uhuru na mamlaka kamili ya kujitawala pasi na kuwepo uingiliaji wa maajinabi."
Siku ya Ijumaa, Mohammed al-Menfi alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Urais la Libya huku Abdulhamid al-Dabaiba akichaguliwa kuwa waziri mkuu katika zoezi ambalo limesimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Uongozi mpya wa Libya utaitayarisha nchi hiyo kwa ajili ya uchaguzi wa bunge utakaofanyika Disemba 24. Aidha uongozi mpya unatarajiwa kuwahakikishia Walibya kuwa wameshirikishwa katika utawala.
Ni vyema kuashiria kuwa, kwa muda mrefu Libya imekuwa na serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, ya Jenerali Haftar, na nyingine ni Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Haftar anapata uungaji mkono wa kijeshi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Ulaya.
Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) lilishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.
Tangu wakati huo, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imekuwa ikishuhudia vita vya ndani na machafuko ambayo yameharibu na kuvuruga kabisa maisha ya raia wa nchi hiyo na kutishia kutokea maafa ya kibinadamu.