Mej. Jen. Baqeri: Ustawi wa Iran umeyaingiza kiwewe madola makubwa
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo kwamba madola makubwa duniani yameingiwa na kiwewe na wahaka kutokana na uwezo, ustawi na pia nafasi ya kistratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Meja Jenerali Mohammad Baqeri ameyasema hayo leo katika ujumbe maalumu alioutuma kwa munasaba wa kuwadia mwaka wa 42 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika ujumbe huo ameongeza kuwa, madola makubwa duniani yamekuwa yakifuatilia kwa karibu uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hayana budi ila kuwa watazamaji tu wa Iran ambayo ni nchi yenye uwezo mkubwa kimataifa.
Meja Jenerali Baqeri amesema madola hayo makubwa yatake yasitake, yanapaswa kujitayarisha kukubali mlingano mpya wa nguvu kieneo ambapo Iran na watu wa Iran ni mhimuli mkuu wa nguvu hiyo.
Kesho Iran itaadhimisha mwaka wa 42 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yaliongozwa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.
Ikumbukwe kuwa 12 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsia sawa na Februari Mosi 1979, Imam Khomeini (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka kadhaa. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia.
Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, yaani Februaria 11 1979, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili. Kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi". Kila mwaka hufanyika sherehe kubwa kwa mnasaba wa kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.