May 10, 2016 05:13 UTC
  • Dehqan: Katu Iran haitasita kufanyia majaribio makombora

Wizara ya Ulinzi ya Iran imesema katu Jamhuri ya Kiislamu haitachoka kujiimarisha kiulinzi na kusisitiza kuwa haina nia au mpango wa kuacha kuyafanyia majaribio makombora yake.

Akizungumza jana Jumatatu, Brigedia Jenerali Hussein Dehqan Waziri wa Ulinzi wa Iran, alisema nchi hii haijawahi kufuata mkondo wa kutekeleza hujuma yoyote ile na kwamba kujiimarisha kiulinzi na kijeshi ni kwa ajili ya kujihami na kuzima chokochoko za maadui.

Brigedia Jenerali Dehqan kadhalika amekosoa Marekani na Saudi Arabia kwa kueneza anga ya taharuki na wasi wasi juu ya kujiimarisha kiulinzi Jamhuri ya Kiislamu. Amesema madola ya kibeberu yamekuwa yakieneza chuki dhidi ya Iran ili kuhalalisha uwepo wao katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Iran amepuulizia mbali taarifa iliyochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, Iran hivi karibuni ilifanyia majaribio kombora la balistiki lenye uwezo wa kupiga masafa ya kilomita 2,000 na kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa. Naibu Mkuu wa Majeshi ya Iran Brigedia Jenerali Ali Abdollahi jana Jumatatu alinukuliwa na shirika la habari la Tasnim akisema kuwa: " Wiki mbili zilizopita, tulifanyia jaribio kombora lenye uwezo wa kuruka kilomita 2,000 na lenye mwanya wa kasoro, (margin of error) wa mita nane."

Licha ya Iran kusisitiza mara kwa mara kuwa lengo la kufanyia majaribio makombora yake ni kwa ajili ya kujiimarisha kiulinzi, lakini nchi za Magharibi hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimekuwa zikikosoa majaribio hayo na kudai kuwa eti yanakiuka azimio nambara 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya mapatano ya nyuklia ya Iran yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.

Tags