Mar 12, 2021 02:42 UTC
  • Iran yapokea shehena za chanjo za Corona kutoka India na Cuba

Shehena ya kwanza ya makumi ya maelfu ya dozi za chanjo ya kubaliana na ugonjwa wa Covid-19 kutoka India iliwasili hapa nchini Iran jana Alkhamisi.

Kianoush Jahanpour, Msemaji wa Taasisi ya Kusimamia Chakula na Dawa ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu imepokea dozi laki moja na 50 elfu (150,000) za chanjo ya Corona ya COVAXIN iliyozalishwa na Taasisi ya Bharat Biotech ya India.

Hii ni shehena ya kwanza ya chanjo ya kupambana na maradhi ya kuambukiza ya Covid-19 kuwasili hapa nchini kutoka India.

Kadhalika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hiyo jana ilipokea shehena ya kwanza ya chanjo ya Corona kutoka Cuba iliyosheheni dozi laki moja (100,000). Shehena hiyo iliwasili jana alasiri katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Imam Khomeini hapa mjini Tehran.

Iran inasema karibuni itakuwa mzalishaji mkubwa wa chanjo ya Corona duniani

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, Iran ilipokea shehena nyingine iliyokuwa imebeba dozi 250,000 za chanjo ya Corona ya shirika la madawa la Sinopharm la China. Kadhalika Iran imeshapokea shehena kadhaa za chanjo ya kupambana na virusi vya Corona ya Sputnik V ya Russia.

Wataalamu na wanasayansi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wako mbioni kutengeneza chanjo za Corona za ndani ya nchi na pia kwa ushirikiano na mataifa mengine rafiki.

Tags