Jeshi la IRGC kupokea nyambizi zilizoundwa hapa nchini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i68182-jeshi_la_irgc_kupokea_nyambizi_zilizoundwa_hapa_nchini
Mkuu wa Shirika la Viwanda vya Baharini la Wizara ya Ulinzi na Lojistiki za Vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili litaanza kutengeneza nyambizi nyepesi na za wastani mwaka huu mpya wa Kiirani wa 1400 ulioanza jana Machi 21.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2021 06:36 UTC
  • Jeshi la IRGC kupokea nyambizi zilizoundwa hapa nchini

Mkuu wa Shirika la Viwanda vya Baharini la Wizara ya Ulinzi na Lojistiki za Vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili litaanza kutengeneza nyambizi nyepesi na za wastani mwaka huu mpya wa Kiirani wa 1400 ulioanza jana Machi 21.

Admeri Amir Rastegari amesema hayo leo Jumatatu katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, nyambizi hizo zitakazozalishwa na wataalamu wa humu nchini zitakabidhiwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).

Ameeleza bayana kuwa, utegemezi wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa madola ajinabi katika sekta ya majini hii leo umepungua kutoka asilimia 70 hadi 20. 

Amebainisha kuwa, ili taifa hili liwe na uwezo wa kujilinda na chokochoko za maadui sambamba na kulinda maslahi yake ya baharini, sharti liimarishe uwezo wa vikosi vyake vya baharini viweze kukabiliana na uvamizi wa maadui.

Admeri Rastegari

Mwaka juzi 2019 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua nyambizi ya kisasa iliyoundwa hapa nchini ambayo ina uwezo wa kusheheni makombora ya cruise. Kabla ya hapo pia, Iran ilizindua nyambizi mbili za Ghadir ambazo zina uwezo wa kurusha makombora kutoka chini ya bahari.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imeweza kuzindua nyambizi kadhaa za kisasa zilizoundwa humu nchini kama vile Qaem, Nahang, Tareq, Fateh na Sina.

Moja ya nyambizi za Iran