Iran: Misimamo inayochukuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ni haribifu
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna amesema kuhusu kauli aliyotoa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwamba, kuendelea kuchukua misimamo ya kisiasa badala ya kiufundi, hakujengi bali kunabomoa.
Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna ameyasema hayo kufuatia matamshi ya hivi karibuni aliyotoa Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA na kusisitiza kuwa, mahojiano ya aina hiyo anayofanya mara kwa mara Grossi yanazidi kuchafua zaidi tu itibarii ya wakala huo wa atomiki mbele ya Iran na Wairan.
Kazem Abadi aidha amesema, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanakabiliwa na matatizo na masuala tata kadhaa, hivyo hakuna haja ya kuyatatiza zaidi kwa misimamo ya ajabu kama aliyochukua mkurugenzi mkuu wa IAEA.
Balozi na mwakilkishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna ametanabahisha kuwa haifai kutumia madai yanayohusiana na kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita kama kisingizio cha kutetea kosa la makusudi la kukwepa kushughulikia matatizo muhimu ya nyuklia likiwemo la hali ya kinyuklia ya utawala wa Israel.
Katika mahojiano aliyofanyiwa hivi karibuni na gazeti la kila wiki la Newsweek linalochapishwa nchini Marekani, Rafael Grossi,Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki alidai kuwa, kuna ulazima wa kufanyika majadiliano ya kina na kiufundi, ili kuelewa mahali yalipo madini ya urani nchini Iran ambayo hayajatangazwa na kwamba suala hilo linahusiana kikamilifu na mustakabali wa makubaliano ya nyuklia.../