China na Iran kusaini mkataba wa ushirikiano
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China leo Jumamosi zinatia saini mkataba wa ushirikiano wa miaka 25 huku nchi mbili zikiadhimisha miaka 50 tokea zianzishe uhusiano.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi yuko nchini Iran kwa ajili ya kutia saini mkataba huo. Amongeza kuwa: "Safari hii inafanyika wakati huu wa kuwadia mwaka wa 50 wa kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Iran na China. Katika safari hii mkataba wa ushirikiano wa nchi mbili katika muda wa miaka 25 utatiwa saini."
Khatibzadeh ameongeza kuwa, katika safari hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa China atakutana na maafisa wa ngazi za juu wa Iran na kwamba nukta muhimu zaidi ya safari hiyo ni kutiwa saini mkataba huo wa ushirikiano wa nchi mbili ambazo sasa zina uhusiano wa kistratijia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mapatano hayo ya ushirikiano wa Iran na China yameainisha ramani kamili ya njia na kuongeza kuwa: "Msingi maalumu wa mapatano hayo ni ushirikiano wa kiuchumi." Aidha amesema mapatano hayo yanahusu ushirikiano wa nchi mbili katika sekta mbali mbali na kushiriki Iran katika ule mpango wa China wa uchukuzi wa kimataifa wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja'. Hali kadhalika mapatano hayo yanajumuisha pia ushirikiano katika sekta za utamaduni na habari.
Rasimu ya mkataba wa ushirikiano wa miaka 25 baina ya China na Iran iliidhinishwa na Baraza la Mawaziri la Iran hivi karibuni na kwa msingi huo Wizara ya Mambo ya Nje iliamrishwa ikamilishe mchakato wa utiwaji saini mkataba huo.
Mkataba huo unajumuisha ushirikiano katika sekta za kisiasa, kiusalama, kiulinzi, kiutamaduni, kilimo, kiuchumi, kisayansi, kitalii, mafuta na gesi, teknolojia ya habari na mawasiliano, biashara na afya.