Namaki: Iran itakuwa moja ya vituo vikuu vya uzalishaji wa chanjo duniani
Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran amesema kuwa, kutokana na hima ya vijana wa nchi hii, Iran itakuwa moja ya wazalishaji wakuu wa chanjo ya corona ulimwenguni.
Daktari Saeed Namaki alisema hayo jana Alkhamisi katika maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Sherehe ya Bendera na Kupeperushwa Bendera ya Iran katika urefu wa mita 250 katika Bustani ya Kitabu jijini Tehran na kuongeza kuwa, historia ya Iran imegawika katika sehemu tatu, kabla ya Uislamu, baada ya Uislamu na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na si sahihi kutofikiria vipindi viwili vya huko nyuma na kufikiria tu kipindi hiki cha tatu.
Vile vile amesema, taifa kubwa la Iran kwa kutegemea ustaarabu na utamaduni wake wa karne nyingi, bado limeshikamana na ada na desturi zake zisizopingana na Uislamu na ndio maana sikukuu ya jadi ya Nairuzi na sikukuu mbili za Idul Fitr na Mfunguo Tatu zina nafasi kubwa humu nchini.
Katikati ya mwezi ulioisha wa Machi, Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran alitangaza kuwa chanjo za corona zilizotengenezwa humu nchini zitaanza kutumika katika soko la ndani karibuni hivi.
Daktari Saeed Namaki alisema, kuanzia mwezi huu wa Aprili 2021, chanjo zilizotengenezwa humu nchini zitaanza kutumika kwa ajili ya wananchi wote.
Alisema, mashirika ya Iran ya COVIran Barakat, Pasteur, Razi CovPars na Fakhra pamoja na taasisi nyinginezo, zitazalisha chanjo za Kiirani zenye ubora, ambazo zitauzwa katika soko la dunia.
Dakta Namaki wakati huo alisema, hivi sasa asilimia 80 ya chanjo zilizotengenezwa duniani zinatumika katika nchi saba pekee.