Baraza la Kukurubisha Madhehebu lapongezwa kwa kuimarisha umoja baina ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i68586-baraza_la_kukurubisha_madhehebu_lapongezwa_kwa_kuimarisha_umoja_baina_ya_waislamu
Katibu Mkuu wa Harakati ya Umma ya Lebanon ametilia mkazo nafasi ya Baraza la Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu katika kuimarisha umoja baina ya Waislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2021 09:41 UTC
  • Baraza la Kukurubisha Madhehebu lapongezwa kwa kuimarisha umoja baina ya Waislamu

Katibu Mkuu wa Harakati ya Umma ya Lebanon ametilia mkazo nafasi ya Baraza la Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu katika kuimarisha umoja baina ya Waislamu.

Sheikh Abdullah al Jabri, ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo aliyofanya na Katibu Mkuu wa Baraza la Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu Hujjatul Islam Hamid Shahryari na akaongeza kuwa, baraza hilo limeonyesha njia na muelekeo wa kuleta umoja kwa ajili ya kukabiliana na changamoto.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut wawili hao walisisitiza pia kuhusu umuhimu wa utoaji elimu katika maendeleo ya umma wa Kiislamu na udharura wa kueneza na kusamabaza elimu hiyo kwa ajili ya kupambana na ujinga; na kuongeza maarifa na uelewa wa elimu mbalimbali ili kukitaalamisha kizazi kijacho na kujenga ustaarabu wa kiutu.

Hujjatul Islam Hamid Shahryari 

Nukta nyingine iliyotiliwa mkazo katika mazungumzo kati ya Sheikh Abdullah al Jabri na Hujjatul Islam Hamid Shahriyari ni kuelekezwa kwa nguvu sawa jitihada za kila upande na uwezo wa umma wa Kiislamu kwa ajili ya kupigania na kutetea haki zake, kukabiliana na changamoto katika nyuga tofauti hususan katika suala la Palestina pamoja na kutetea haki za taifa hilo na matukufu ya Kiislamu ya mji wa Quds, kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu na mahali ilipoanzia safari ya Miraji ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Viongozi hao wamesisitiza pia kuhusu umuhimu wa kuelekeza nguvu zote za umma wa Kiislamu katika kukabiliana na ugaidi wa ukufurishaji ambao unachafua na kuharibu sura ya Uislamu halisi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu Hujjatul Islam Hamid Shahryar, aliwasili mjini Beirut siku ya Jumatatu kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Lebanon pamoja na kuhudhuria hafla kadhaa nchini humo.../