Araqchi: Kuondolewa vikwazo na Marekani ndio hatua ya kwanza ya kufufua JCPOA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema, kuondolewa vikwazo na Marekani ndio hatua ya kwanza ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Sayyid Abbas Araqchi ameyasema hayo leo katika kikao cha kamati ya pamoja ya JCPOA kilichofanyika kwa njia ya mawasiliano ya video, kikiongozwa na Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu anayehusika na sera za pamoja za nje na za usalama za Umoja wa Ulaya kwa niaba ya Mkuu wa Sera za Nje wa umoja huo Josep Borrell na kuhudhuriwa pia na wawakilishi wa China, Ufaransa, Ujerumani, Russia, Uingereza na Iran katika ngazi ya manaibu na wakurugenzi wa kisiasa wa wizara za mambo ya nje za nchi hizo.
Araqchi, ambaye ndiye aliyeongoza ujumbe wa Iran katika kikao hicho, ameashiria misimamo mikuu ya Iran akisisitiza kuwa, kuondolewa vikwazo na Marekani ndio hatua ya kwanza ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Aidha akasema, mara tu vikwazo vitakapoondolewa na kuthibitika athari za hatua hiyo, Iran itasitisha hatua za ufidiaji za nyuklia ilizokuwa imetekeleza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema, kurejea Marekani katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA hakuhitaji mazungumzo yoyote, kwa sababu njia inayopasa kufuatwa na Marekani katika suala hilo iko wazi kabisa na akaofafanua kuwa, kama Marekani ilivyojiondoa katika mapatano ya JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo haramu, inaweza kwa njia hiyo hiyo pia kurejea kwenye makubaliano hayo na kuhitimisha uvunjaji wake wa sheria.
Katika kikao chao hicho, nchi wanachama wa JCPOA zimeashiria maafa yaliyosababishwa na Marekani kujitoa katika JCPOA na kusisitiza juu ya namna Iran itakavyonufaika na haki zake katika makubaliano hayo na umuhimu wa kutopotezwa muda katika suala hilo.
Mwishoni mwa mazungumzo yao, wawakilishi wa nchi wanachama wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA wamesisitiza haja ya kila upande kutekeleza majukumu yake na kukubaliana kukutana tena Jumanne ijayo ili kuendeleza mashauriano kwa ajili ya uchukuaji hatua kuhusiana na kuondolewa vikwazo na kusitishwa hatua za nyuklia kupitia kundi la wataalamu husika.../