Iran yawasilisha malalamiko kwa IAEA kuhusu ugaidi wa kinyuklia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha malalamiko rasmi kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu tukio la kigaidi katika mfumo wa usambazaji umeme wa kituo cha urutubishaji urani cha Natanz hapa nchini.
Katika barua kwa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Kazem Gharibabadi, Balozi na Mwakilishi wa Iran katika IAEA mjini Vienna, amesema hujuma hiyo ya kuvuruga mfumo wa umeme katika kituo cha urutubishaji cha Natanz ni mfano wa ugaidi wa kinyuklia.
Jumapili iliyopita kuuliripotiwa tukio katika sehemu moja ya mtandao wa kusambaza umeme katika kituo cha kurutubisha madini ya urani cha Shahid Ahmadi Roshan huko Natanz lakini kwa bahati nzuri tukio hilo halikusababisha maafa ya binadamu wala kuvuja kwa mionzi ya nyuklia.
Akizungumzia tukio hilo la kigaidi hivi karibuni, Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran alisema kwamba ugaidi wa kinyuklia ambao umetokea katika kituo cha urutubishaji urani cha Natanz ni thibitisho la wazi la kushindwa wapinzani wa ustawi wa kiviwanda na kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kuzuia maendeleo makubwa ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Naye Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza Jumatatu asubuhi katika kikao cha Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) pia aliashiria tukio hilo la Natanz na kusisitiza udharura wa kulindwa vizuri usalama wa taasisi na wanasayansi wa nyuklia katika mazingira haya tata.
Magazeti ya Israel yamesema hujuma hiyo ya uvurugaji katika kituo cha Natanz imetekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.