Iran yalalamikia ukiukwaji wa haki za Wairani barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69050-iran_yalalamikia_ukiukwaji_wa_haki_za_wairani_barani_ulaya
Iran imelalamikia vikali ukiukwaji wa haki za Wairani katika nchi za Umoja wa Ulaya na imetangaza kumteua ripota maalumu wa kuchunguza hali mbaya ya wafungwa Wairani katika magereza ya Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 14, 2021 22:51 UTC
  • Iran yalalamikia ukiukwaji wa haki za Wairani barani Ulaya

Iran imelalamikia vikali ukiukwaji wa haki za Wairani katika nchi za Umoja wa Ulaya na imetangaza kumteua ripota maalumu wa kuchunguza hali mbaya ya wafungwa Wairani katika magereza ya Ulaya.

Ali Baqeri Kani, Katibu wa Kitengo cha Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama ya Iran amemuandikia barua Jeppe Tranholm-Mikkelsen, Katibu Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya ambapo amebainisha namna haki za raia wa Iran zinavyokiukwa barani Ulaya. 

Amekosoa vikali nchi za Umoja wa Ulaya kwa kutowajibika kuhusu kadhia hiyo ya kukiukwa haki za Wairani barani Ulaya. Aidha amezitaka nchi za Ulaya zishirikiane na ripota maalumu wa Iran ambaye atakuwa na jukumu la kuchunguza hali ya wafungwa Wairani barani humo.

Katibu wa Kitengo cha Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama ya Iran aidha ameashiria hatua zilizo dhidi ya ubinadamu za baadhi ya serikali za Ulaya ambapo ametoa mfano wa Ujerumani kukata ushirikiano na shirika la Iran la Armita Teb Novin katika uga wa damu. Aidha ametaja mifano mingine ya kukiukwa haki za Wairani kuwa ni kufariki watoto 31 Wairani waliokuwa wakiugua magonjwa ya MIS na EB kutokana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya ambavyo vilizuia dawa za dharura ziwafikie.

Mtoto anayeugua ugonjwa wa EB

Aidha Baqeri Kani amezikosoa nchi za Ulaya kwa kunyamazia kimya ugaidi wa kiserikali wa utawala wa Marekani hasa mauaji ya Shahidi Qassem Soleimani.

Ali Baqeri Kani, Katibu wa Kitengo cha Haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama ya Iran aliwasilisha barua hiyo ya malalamiko Jumatano mjini Tehran wakati alipokutana na Balozi wa Ureno ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa kiduri wa Baraza la Umoja wa Ulaya.