Rais Rouhani: Kuwa na uhusiano na Uturuki kuna umuhimu mkubwa kwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69060-rais_rouhani_kuwa_na_uhusiano_na_uturuki_kuna_umuhimu_mkubwa_kwa_iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa kidugu na wa kushibamana na Uturuki ikiwa nchi jirani na ya Kiislamu ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa Tehran.
(last modified 2026-08-11T03:40:48+00:00 )
Apr 15, 2021 03:48 UTC
  • Rais Rouhani: Kuwa na uhusiano na Uturuki kuna umuhimu mkubwa kwa Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa kidugu na wa kushibamana na Uturuki ikiwa nchi jirani na ya Kiislamu ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa Tehran.

Rais Rouhani amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki na kusisitiza juu ya udharura wa kustawishwa na kupanuliwa zaidi ushirikiano wa nchi mbili hizo katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kibiashara.

Katika mazungumzo hayo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sa8mbamba na kutoa mkono wa kheria na baraka kwa serikali na wananchi wa Uturuki kwa mnasaba wa kuwadia mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ameeleza kuwa, uhusiano wa nchi mbili hizo umejengeka juu ya msingi wa udugu na urafiki na kwamba, kupanuliwa zaidi ushirikiano huo kunaweza kuimarisha mashirikiano ya kirafiki na kusaidia kuwa na mchango bora katika matukio ya eneo.

Bendera za taifa za Iran na Uturuki

 

Rais Rouhani ameashiria piia katika mazungumzo yake hayo na Rais Erdogan kuhusu harakati na chokochoko za kigaidi za utawala haramu wa Israel katika eneo pamoja na ugaidi wa kinyuklia na kusisitiza kwamba, ushirikiano wa nchi za eneo kwa ajili ya kudhamini usalama na amani ni jambo la dharura.

Kwa upande wake Rais Recep Tayyip Erdoğan sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa serikali na wananchi wa Iran kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani amesema kuwa, nchi yake ina azma na irada thabiti ya kupanua zaidi ushirikiano wake na Tehran katika nyanja mbalimbali.