Araqchi: Tumeingia kwenye mkondo sahihi wa mazungumzo ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69160-araqchi_tumeingia_kwenye_mkondo_sahihi_wa_mazungumzo_ya_jcpoa
Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema baada ya kikao cha kamati ya pamoja ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA mjini Vienna, Austria kwamba inavyoonekana sasa tumeingia katika mkondo sahihi wa mazungumzo hayo baada ya siku kadhaa za majadiliano mazito ingawa hata hivyo bado kuna safari ndefu mbele yetu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2021 22:27 UTC
  • Araqchi: Tumeingia kwenye mkondo sahihi wa mazungumzo ya JCPOA

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema baada ya kikao cha kamati ya pamoja ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA mjini Vienna, Austria kwamba inavyoonekana sasa tumeingia katika mkondo sahihi wa mazungumzo hayo baada ya siku kadhaa za majadiliano mazito ingawa hata hivyo bado kuna safari ndefu mbele yetu.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la FARS ambalo limemnukuu Araqchi akisema pia kuwa, bado ni mapema kutabiri matokeo; timu za wataalamu zinaendelea na kazi yao nzito ya kuweka wazi maudhui muhimu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa alisema hayo jana jioni na kuongeza kuwa, inaonekana kuna maelewano mapya yanafikiwa. Mazungumzo hivi sasa yamefikia hatua ambayo pande husika zinaweza kuanza kwenye hati inayokubaliwa na wote. Ujumbe wa Iran umeandaa hati yake na kuwaonesha wote.

Kikao cha kamisheni ya pamoja na mapatano ya nyuklia ya JCPOA kilifanyika jana jioni huko Vienna, mji mkuu wa Austria.

Enrique Mora, naibu wa mkuu wa siasa za kigeni wa Umoja wa Ulaya, wajumbe wa Iran, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, China na Russia wameshiriki kwenye kikao hicho.

Baada ya kikao hicho, Mora ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, maendeleo yaliyojitokeza katika mazungumzo ya JCPOA hayakupatikana kiurahisi. Hivi sasa kuna kazi ndogondogo nyingi zinapaswa kufanywa. Hata hivyo siri ya mafanikio yetu ni kwamba pande zote zinataka Marekani irejee kwenye mapatano hayo na kila mmoja aheshimu vipengee vyake vyote.