Hatima ya JCPOA kupitia mazungumzo ya Vienna
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69214-hatima_ya_jcpoa_kupitia_mazungumzo_ya_vienna
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua maamuzi na kutekeleza hatua za kujibu mapigo, kutokana na Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kufuata sheria ya “hatua ya kimkakati kwa ajili ya kuondolewa vikwazo na kulindwa maslahi ya taifa la Iran”.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2021 07:10 UTC
  • Hatima ya JCPOA kupitia mazungumzo ya Vienna

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua maamuzi na kutekeleza hatua za kujibu mapigo, kutokana na Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kufuata sheria ya “hatua ya kimkakati kwa ajili ya kuondolewa vikwazo na kulindwa maslahi ya taifa la Iran”.

Lakini wakati huohuo, Iran imeonyesha pia subira ya kistratejia ili kuhakikisha makubaliano ya JCPOA, yakiwa ni hati ya kujenga hali ya kuaminiana, yanaendelea kulindwa. Ni kwa kufuata muelekeo huo, siku ya Alkhamisi iliyopita, kikao cha kamati ya pamoja ya JCPOA katika ngazi ya wakurugenzi na wakuu wa kisiasa wa Iran na kundi la 4+1 kilifanyika katika hoteli kuu ya mji wa Vienna, kwa lengo la kuufanyia tathmini jumla mwenendo wa mazungumzo. Mashauriano baina ya wataalamu pia yanaendelea kufanyika kati ya pande mbili na baina ya pande kadhaa; na masuala husika yanajadiliwa katika majopokazi mawili ya nyuklia na vikwazo.

Mazungumzo hayo yanafuatiliwa kwa karibu na duru za habari na za kisiasa; na kwa ujumla kuna mtazamo chanya na wa kutia matumaini kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo. Lakini pamoja na hayo, kuna mistari myekundu na mambo ya kuzingatiwa pia kuhusiana na mazungumzo ya Vienna.

Kikao cha kamati ya pamoja ya JCPOA kikiendelea mjini Vienna

Kimsingi, kuna malengo matatu muhimu ya kuzingatiwa katika mazungumzo ya sasa ya JCPOA:

La kwanza ni kwamba, muelekeo unaofuatwa katika mazungumzo inapasa ufahamike wazi na uwe unahusiana na masuala ya kiufundi tu ya JCPOA na kuondolewa kikamilifu vikwazo ilivyowekewa Iran. Na kwa muktadha huo, kinachopasa kufanywa na upande wa pili kinajulikana na kiko wazi kabisa.

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa, mbali na kuashiria kwamba makubaliano mapya yanaanza kufikiwa huko Vienna na mazungumzo yamekaribia kufika kwenye hatua ya kuridhisha, amesema hivi sasa pande husika zinaifanyia kazi hati ya pamoja.

Kwa ajili hiyo, wawakilishi wa Iran katika mazungumzo wameandaa rasimu ya mapendekezo katika uga wa nyuklia na uondoaji vikwazo na kuiwasilisha kwa pande zingine; na mapendekezo hayo yanaweza kuwa msingi wa kuendeleza mazungumzo na kufikia makubaliano rasmi. Pamoja na hayo, kungali kuna safari ndefu kama alivyotanabahisha pia Araqchi kwamba, “ni mapema bado kutabiri matokeo.”

Sayyid Abbas Araqchi

Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ameandika yafuatayo katika ukurasa wake wa Twitter: “Upigaji hatua katika mazungumzo ya JCPOA haujapatikana kirahisi. Sasa yanahitaji kushughulikiwa masuala ya ndani zaidi; lakini msingi wa mafanikio yetu ni pande zote husika kutaka Marekani irudi kwenye JCPOA na kutekeleza makubaliano ya nyuklia.”

Lakini lengo la pili linahusu kuendelea na kukamilishwa mazungumzo ya pande mbili na baina ya pande kadhaa, na pia mashauriano ya kiufundi ambayo yameendelea katika siku chache zilizopita. Endapo itahitajika, kamati ya pamoja ya JCPOA itafanya tena kikao kingine, lakini kwa msisitizo kwamba, mazungumzo yenyewe yasiwe ya urefusho. Mazungumzo ya urefusho yanaharibu vibaya nia ya upande wa pili na kuondoa hali ya kuaminiana. Kwa hivyo inapasa kuangalia kama kasi iliyopo ni ya kukubalika kwa ajili ya kufikia mwafaka; vyenginevyo Iran haitakuwa na sababu ya kuendelea kufanya mazungunmzo.

Kazem Gharib Abadi, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna ametilia mkazo nukta hiyo kwa kusisitiza kwamba: “Mwongozo unaofuatwa na timu ya mazungumzo ya Iran ni msingi ulioainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo ndiyo sera ya mfumo wa utawala kuhusiana na suala hilo.”

Na ama lengo la tatu ni kuwepo hakikisho la kuondolewa kikamilifu vikwazo na kuzipima hatua na utendaji wa Marekani na Ulaya katika suala hilo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, itarejea tena katika utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya Marekani kuondoa vikwazo vyote kivitendo, si kwa maneno matupu au kwa maandishi tu; na uondolewaji huo kupimwa na kuthibitishwa na Iran.

Kusema kweli uendelezaji wa makubaliano ya JCPOA kwa sura ya kutekelezwa na upande mmoja tu, umeyaumiza mno maslahi na haki za taifa la Iran; na kwa hiyo inapasa suala hilo lifidiwe. Kwa sababu hiyo, msimamo wa Iran katika mazungumzo ya Vienna uko wazi kabisa. Tajiriba imeonyesha kuwa “mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo” hayasaidii kwa namna yoyote ile kufungua mafundo yaliyozonga mapatano ya JCPOA…/