Rabie: Iran haitalegeza msimamo katika mapatano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69250-rabie_iran_haitalegeza_msimamo_katika_mapatano_ya_jcpoa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitalegeza msmamo zaidi ya yale yaliyomo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na madola makubwa duniani.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Apr 20, 2021 22:03 UTC
  • Rabie: Iran haitalegeza msimamo katika mapatano ya JCPOA

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu haitalegeza msmamo zaidi ya yale yaliyomo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na madola makubwa duniani.

Ali Rabiei msemaji wa serikali ya Iran aliyasema hayo jana Jumanne katika mkutano na waandishi habari huku mazungumzo yakiendelea Vienna, Austria kwa lengo la kuhuisha mazungumzo hayo.

Hii leo duru nyingine ya mazungumzo ya pande husika katika JCPOA inafanyika huko Vienna kwa lengo la kutafuta njia ya kuondoa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na pia hatua ambazo Tehran inapaswa kuzichukua ili kurejea kikamilifu katika utekelezaji wa ahadi zake katika mapatano hayo.

Akijibu swali kuhusu iwapo washiriki katika mazungumzo wameafikiana kuhusu kuandikwa rasimu ya hatua ambazo zitachukuliwa na iwapo Iran ina matumaini ya kuondolewa vikwazo haraka, Rabie amesema: “Kiufundi kuna uwezekano wa kuondolewa vikwazo vyote ambavyo vinakiuka JCPOA na hivyo kuhuisha mapatano hayo kikamilifu. Tuna matumaini kuwa tutafikia malengo kusudiwa katika mazungumzo.”

Serikali ya Trump mwezi Mei mwaka 2018 ilijitoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo ya kimataifa na kisha ikitekeleza mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ili kuwaweka chini ya mashinikizo wananchi wa Iran na kuilazimisha Tehran ikubali matakwa yake yaliyo kinyume cha sheria. Mazungumzo hayo ya Vienna yanajumuisha Iran na nchi zilizosalia katika JCPOA ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.