Rouhani: Iran haiwezi kusitisha ustawi wake kutokana na vikwazo au mashinikizo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran haiwezi kusitisha mchakato wake wa ustawi kutokana na vikwazo na mashinikizo.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo Alhamisi alipozindua miradi kadhaa ya maendeleo ya Wizara ya Jihadi ya Kilimo. Akizindua miradi hiyo kwa njia ya video, Rais Rouhani amesema: "Moja kati ya malengo yetu katika uzinduzi wa miradi hii ni kuifahamisha dunia kuwa, mkondo wetu wa ustawi na maendeleo hauwezi kusitishwa kwa vikwazo na mashinikizo." Rais Rouhani amesema pamoja na kuwepo vikwazo na janga la corona, Iran imeweza kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo.
Rais wa Iran amesema miaka minane iliyopita unyunyiziaji maji mashamba ulikuwa umefika hekari milioni 1 na laki mbili lakini kiwango hicho sasa ni hekari milioni mbili na laki nne.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema vikwazo ni dhulma kubwa kwa taifa adhimu la Iran na kuongeza kuwa, wakati tutaona upande wa pili uko tayari kutekeleza sheria na kanuni, sisi nasi pia tutachukua hatua wakati huo huo.
Aidha amesema yeye kama rais wa nchi hatachelewa hata dakika moja kuchukua hatua za kulinda haki za watu wa Iiran.