Kiongozi Muadhamu kuhutubu katika Siku ya Kimataifa ya Quds
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu atahutubu kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds.
Hayo yamedokezwa na Nusratullah Lotfi, Kaimu Mkuu wa Baraza la Uratibu wa Uwenezi wa Kiislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa amesema: "Kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu atahutubu Ijumaa Mei 7 saa tano asubuhi kwa saa za Tehran."
Amesema hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu itaruhswa hewani mubashara katika radio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Kati ya televisheni za kimataifa za Iran zitakazorusha hotuba hiyo mubashara ni pamoja na Press TV, Al Alam, Al Kauthar, Iran Press na Hispan TV.
Ikumbukwe kuwa, Imam Khomeini MA Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Kimataifa ya Quds.
Waislamu na wapenda haki wamekuwa wakifanya maandamano katika pembe mbalimbali za dunia kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds, na kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi na kikatili zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 katika aghalabu ya maeneo ya dunia hakutafanyika mijumuiko hadharani katika Siku ya Kimataifa ya Quds bali kutakuwepo zaidi na harakati katika mitandao ya kijamii zikiwemo hotuba za shakhsia mbali mbali.