IRGC: Mienge ya Intifadha na Muqawama ya Palestina haitazimika
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza kuwa mienge ya Intifadha na Muqawama ya Palestina haitazimika.
Katika taarifa iliyotoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Sepah imesema, siku hiyo ni dhihirisho la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kuihami na kuiunga mkono Palestina na ikabainisha kwamba, Intifadha na Muqawama wa Palestina havitazimika.
Taarifa hiyo ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imebainisha kuwa, zaidi ya miongo minne imepita, tangu ilipochukuliwa hatua ya hekima na ya kistratejia na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) ya kuitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds na kubainisha manifesto ya kuiokoa Palestina.
IRGC imeashiria pia katika taarifa yake hiyo njama za kishetani za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel za kuzusha mpasuko na mfarakano baina ya mataifa ya Kiislamu na ikabainisha kuwa, mipango ya kikhabithi na kijinai ya kufanya mapatano, ukiwemo wa "Muamala wa Karne" itafeli na kugonga mwamba.
Taarifa hiyo ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile imewaenzi na kuwakumbuka mashahidi wa Intifadha ya Palestina pamoja mchango wa Kamanda mwenye hadhi kubwa shahidi Qassem Suleimani katika kufanikisha malengo matukufu ya ukombozi wa Quds tukufu na ikasisitiza kuendeleza njia ya shahidi huyo huku ikikumbusha kwamba: utawala wa Kizayuni uko kwenye mteremko wa kuporomoka na kutoweka.../