Kanani Chafi: Utawala wa Kizayuni ni mradi wa mabeberu wa kuwadhibiti Waarabu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69888-kanani_chafi_utawala_wa_kizayuni_ni_mradi_wa_mabeberu_wa_kuwadhibiti_waarabu
Mkuu wa Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Misri amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ni mradi wa madola ya kibeberu kwa ajili ya kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu katika eneo muhimu na la kiistratijia la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 07, 2021 23:38 UTC
  • Kanani Chafi: Utawala wa Kizayuni ni mradi wa mabeberu wa kuwadhibiti Waarabu

Mkuu wa Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Misri amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ni mradi wa madola ya kibeberu kwa ajili ya kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu katika eneo muhimu na la kiistratijia la Asia Magharibi.

Nasser Kanani Chafi amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, kuanzishwa dola pandikizi la Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi na katika ardhi takatifu za Waislamu ni matunda ya miaka mingi ya uchunguzi na utafiti wa mashirika ya kijasusi na kikoloni ya mabeberu na Uzayuni wa kimataifa.

Ameongeza kuwa, tangu hiyo zamani, dola dhalimu na ghasibu la Kizayuni lilianzishwa na wakoloni na waistikbari wa dunia ili kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu katika eneo hili nyeti na muhimu sana na kwamba kwa miongo mingi sasa, utawala wa Kizayuni unapata uungaji mkono kamili na wa pande zote kutoka kwa Uingereza, Marekani na ulimwengu wa Magharibi.

Nasser Kanani Chafi, Mkuu wa Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Misri

 

Mkuu huyo wa Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Misri pia amesisitiza kuwa, tawala na wananchi wa nchi za eneo hili wanapaswa kuelewa kuwa, kamwe utawala wa Kizayuni hautoishia kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina wala kulifanyia uadui taifa hilo pekee, bali huo ni mradi wa mabeberu wa kuudhibiti ulimwengu mzima wa Kiislamu na Kiarabu, hivyo Waislamu wote na kila mpenda haki duniani, ana jukumu la kuliunga mkono taifa la Palestina na kukabiliana na njama za Uzayuni wa kimataifa. Amesema, hilo si jukumu la Kiislamu na takatifu tu, lakini pia ni jukumu la kibinadamu na kimaadili.

Jana ambayo ilikuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ilikuwa Siku ya Kimtaifa ya Quds ambayo iliadhibitishwa kwa kufana mno katika kona mbalimbali za dunia.