Velayati: Kadhia ya Palestina ni kipaumbele katika sera za kigeni za Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69960-velayati_kadhia_ya_palestina_ni_kipaumbele_katika_sera_za_kigeni_za_iran
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amesema kuwa, kadhia ya Palestina ingali maudhui muhimu na inayopewa kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 09, 2021 22:31 UTC
  • Velayati: Kadhia ya Palestina ni kipaumbele katika sera za kigeni za Iran

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amesema kuwa, kadhia ya Palestina ingali maudhui muhimu na inayopewa kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Dkt. Ali Akbar Velayati, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu ameyasema hayo katika kikao ambacho kimefanyika kwa njia ya intaneti chini ya anuani ya "Siku ya Quds, Siku ya Wanaonyongeshwa". Katika hotuba yake amesema kuwa: "Siku hii kwa hakika ni 'Siku ya Mwenyezi Mungu' na ni wazi kuwa kadhia ya Palestina inapasa iwe kadhia muhimu zaidi na ya kistratijia katika ulimwengu wa Kiislamu."

Dkt. Velayati ameongeza kuwa, katika historia ya mwanadamu hakujawahi kushuhudiwa mkondo mrefu kiasi hiki wa ukatili, unyama na ukaliaji mabavu kama unaofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Aidha amesema mkabala wa jinai hizo, historia imeshuhudia matukio nadra sana kama yanayoshuhudiwa hivi sasa ya jihadi na kusimama kidete makundi ya muqawama na mapambano  dhidi ya Wazayuni maghasibu.

Velayati ameendelea kusema kuwa, mapambano na jihadi ya Wapalestina hatimaye itazaa matunda na kwamba katika mustakabali usio mbali, tutashuhudia kukombolewa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Mji wa Quds

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu aidha amesema ukombozi wa Quds inapasa uwe mhimili wa umoja wa umma wa Kiislamu.

Aidha amesema kitendo cha baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni katika fremu ya "Muamala wa Karne' ni uhaini ambao utapingwa vikali na wananchi.

Katika kikao hicho, Dkt. Velayati ametoa heshima zake kwa mashahidi Wapalestina na wasiokuwa Wapalestina ambao wamepoteza maisha yao katika njia ya kupigania ukombozi wa Quds Tukufu hasa kamanda aliyeuletea ulimwengu wa Kiislamu fahari, shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Aidha ametoa heshima zake pia kwa Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.