Dozi 162,000 za chanjo ya COVID-19 zinatolewa Iran kwa siku
Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki amesema hivi sasa Iran inatoa dozi 162,000 za chanjo ya COVID-19 kwa siku.
Akizungumza na waandishi habari Jumapili, Daktari Namaki amesema kiwango hicho kinatazamiwa kufika dozi 300,000 kwa siku katika kipindi cha siku chache zijazo. Ameongeza kuwa, inatazamiwa kuwa hadi kufikia mwisho wa mwezi Juni watu milioni 14 watakuwa wamepokea chanjo ya COVID-19 nchini Iran.
Aidha amesema katika aghalabu ya nchi za dunia kulishuhudiwa upungufu wa vifaa vya hospitali wakati huu wa janga la COVID-19 hasa baada ya kuibuka aina mpya ya kirusi kutoka Uingereza lakini kwa bahati nzuri Iran haikushuhudia tatizo hilo.
Aidha amesema Iran imeweza kudhibiti maambukizi ya COVID-19 katika miji yote na sasa ni miji mitatu tu ambayo inakabiliwa na kiwango cha juu cha maambukizi.
Wiki iliyopita Mkuu wa Tume ya Utekelezaji Maagizo ya Imam Khomeini (MA) alisema, dozi milioni 30 za chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 iliyotengenezwa na wataalamu wa Kiirani ya COV-Iran Barekat zitakuwa zikizalishwa kila mwezi hapa nchini.
Mohammad Mokhber aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa shehena ya kwanza ya chanjo ya corona aina ya COV-Iran Barekat iliyozalishwa kwa wingi kwa ajili ya matumizi rasmi.
Mbali na COV-Iran Barekat, wataalamu na wanasayansi wa Kiirani wamefanikiwa kutengeneza na kuzalisha aina nyingine kadhaa za chanjo ya COVID-19 ambazo zimesifiwa katika duru za kielimu na kisayansi duniani.