Zarif: Kunahitajika kampeni iliyoratibiwa ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuna haja ya kuwepo kampeni iliyoratibiwa kisheria na ya kisiasa kwa lengo la kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel kieneo na kimataifa.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika kikao cha dharura kilichofanyika kwa njia ya Intaneti cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC cha kuzungumzia Palestina na jinai za utawala wa kibaguzi na kiapathaidi wa Israel.
Katika hotuba yake Zarif amesema: "Wazayuni wanatenda jinai za kinyama zaidi dhidi ya Wapalestina. Ameongeza kuwa: "Wanawake, watoto na wanaume wasio na hatia wameuawa kinyama kwa silaha haribifu na za kisasa zaidi, na nyumba zao zinabomolewa huku wakazi wakiwa ndani." Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kile ambacho utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya dhidi ya Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu, sheria za kibinadamu na sheria za kimataifa.
Ameendelea kusema kuwa leo, mauaji ya watoto Wapalestina yanafanywa baada ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha 'uhusiano wa kawaida' na utawala katili na utendao jinai wa Israel na hivyo imeweza kuthibitika kwamba kuwa na urafiki na utawala huo kutazidisha tu jinai zake.
Zarif amesema lengo la hatua hiyo ya kinafiki ya Israel ya kuanzisha uhusiano na baadhi ya nchi za Kiarabu ni kuibua mgawanyiko katika umma wa Kiislamu na kuwatenga Wapalestina.
Ameendelea kusema kuwa, utawala wa Israel unafahamu lugha ya muqawama na mapambano tu na hivyo Wapalestina ni haki yao kujilinda na kukabiliana na utawala huo wa kibaguzi.
Zarif amesema jinai za Israel dhidi ya Wapalestina zinapaswa kutambuliwa kuwa ni mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu na hivyo hatua za kisheria zinapasa kuchukuliwa dhidi ya utawala huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Iran iko tayari kuweka kando hitilafu zake na nchi zingine kwa lengo la kuunga mkono haki za Wapalestina kwa njia halali na za kisheria.