Velayati: Iran itaendelea kuunga mkono taifa la Palestina
Mshauri mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema kwamba Waislamu wote ulimwenguni wana jukumu la kutetea na kuwaunga mkono Wapalestina wanaokandamizwa kila uchao na utawala wa kigaidi wa Israel. Akisisitiza suala hilo, Ali Akbar Velayati amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kutetea na kuwaunga mkono Wapalestina bila uoga wowote.
Amesema Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikitetea haki za taifa hilo katika miaka iliyopita na kwamba itaendelea kutetea haki hizo kwa nguvu zake zote katika siku na miaka ijayo. Veyalati alitoa sisitizo hilo katika mazungumzo yake ya simu hapo jana Jumapili na Ziyad an-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami.
Dr. Ali Akbar Velati ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mweamko wa Kiislamu amelaani vikali mashambulio ya kinyama yanayofanywa hivi sasa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Waplestina wasio na hatia na hasa wanawake na watoto, na kusema kuwa, kwa mujibu wa ahadi ya Mwenyezi Mungu, hatimaye ushindi wa mwisho utakuwa ni wa Wapalestina kwa kukombolewa ardhi zao zote zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa kibaguzi.
Utawala wa Israel unaendelea kuushambulia kinyama na bila huruma Ukanda wa Gaza kwa siku ya nane mfululizo. Velayati amesema licha ya unyama na ukatili wote unaofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, lakini ulimwengu unashuhudia wazi namna mashujaa wa Palestina wanavyopambana kiujasiri dhidi ya adui Mzayuni.
Ameeleza matumaini yake kuwa siku itafika ambapo ulimwengu utashuhudia kukombolewa kwa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel na hivyo kuwapa wakimbizi wa Kipalestina fursa ya kurejea katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na walowezi wa Kizayuni na Kiyahudi.
Kwa upande wake Nakhalah amesifu msimamo maalumu na wa kishujaa wa Ayatullah Khamenei na kusema kuwa hakuna nchi nyingine yoyote duniani ambayo imekuwa na msimamo kama huo.