Salami: Iran itaendelea kuunga mkono taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i70342-salami_iran_itaendelea_kuunga_mkono_taifa_la_palestina
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami amesema Iran itaendelea kuunga mkono taifa la Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2021 03:29 UTC
  • Salami: Iran itaendelea kuunga mkono taifa la Palestina

Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami amesema Iran itaendelea kuunga mkono taifa la Palestina.

Akihutubu katika mjumuiko wa kuunga mkono taifa la Palestina mjini Tehran Jumatano, Salami amepongeza mapambano shupavu ya Wapalestina mkabala wa hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema zaidi ya thuluthi mbili ya miji ya utawala wa Kizayuni imeshambuliwa kwa maroketi ya Wapalestina kutokea Ghaza na hivyo Wazayuni hawakuwa na pa kukimbilia. Amesema ngao ya makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeshindwa kukabiliana na maelfu ya makombora ya Wapalestina.

Kamanda Mkuu wa IRGC amesema Waisraeli wamekerwa sana na mwamko mkubwa katika harakati za mapambano ya Palestina. Aidha amesema kushindwa Israel ni alama ya kushindwa Marekani na kuongeza kuwa, leo kadhia ya Palestina ni kadhia ya dunia nzima. Amesema Wamarekani na Waisraeli wanakabiliwa na hali ngumu kwani iwapo watasitisha vita Ghaza watakuwa wamefeli na iwapo wataendeleza vita watapata pigo.

Maandamano ya wakazi wa Tehran ya kuunga mkono Wapalestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Meja Jenerali Hossein Salami amesema Israel imepata pigo la kudumu baada ya kiwanda chake cha makombora kulengwa na baada ya hapo kiwanda chake cha kusafisha mafuta cha Haifa kikateketea moto. Matukio hayo yalijiri baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusika katika kuvuruga mitambo ya kituo cha nyuklia cha Iran cha Natanz.