Zarif: Kuendelezwa vikwazo vya Trump kama silaha katika mazungumzo, hakukubaliki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i70394-zarif_kuendelezwa_vikwazo_vya_trump_kama_silaha_katika_mazungumzo_hakukubaliki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaumu kitendo cha Marekani ya kuendelea na vikwazo haramu na visivyo na chembe ya ubinadamu vilivyowekwa na Donald Trump dhidi ya taifa la Iran na kusema kuwa kitendo hicho hakikubaliki hata kidogo.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
May 21, 2021 08:27 UTC
  • Zarif: Kuendelezwa vikwazo vya Trump kama silaha katika mazungumzo, hakukubaliki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaumu kitendo cha Marekani ya kuendelea na vikwazo haramu na visivyo na chembe ya ubinadamu vilivyowekwa na Donald Trump dhidi ya taifa la Iran na kusema kuwa kitendo hicho hakikubaliki hata kidogo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika mazungumzo ya simu na Josep Borrel, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ambapo mbali na kumshukuru kwa juhudi zake na wenzake amesema kuwa, kuendelezwa ugaidi wa kiuchumi wa Marekani katika kipindi cha miezi mitano ya tangu kuingia madarakani Joe Biden ni uvunjaji wa wazi wa ahadi za nchi hiyo.

Zarif amesisitiza kuwa, kitendo cha serikali ya Joe Biden huko Marekani cha kuendeleza vikwazo haramu na visivyo na ubinadamu vya Trump dhidi ya taifa la Iran kama silaha ya mazungumzo, hakikubaliki kabisa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemtaka rais wa Marekani achukue maamuzi sahihi na asirudie makosa ya marais waliotangulia wa nchi hiyo.

Rais wa Marekani, Joe Biden

Kikao cha nne cha kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA cha wawakilishi wa Iran na wa kundi la 4+1 linaloundwa na Ujerumani, Ufaransa, China, Russia na Uingereza, kilimalizika Jumatano jioni mjini Vienna Austria huku pande husika zikisema luwa, kumepigwa hatua nzuri katika mazungumzo hayo. 

Iran inasema, Marekani lazima irejee katika hali iliyokuwa nayo baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaani iondoe kwanza vikwazo vyote ilivyoiwekea kidhulma Iran baada ya kufikiwa makubaliano hayo, na baada ya Tehran kuhakikisha Marekani imerejea kikamilifu kwenye mapatano hayo, ndipo itaanza kutekeleza kikamilfu vipengee vya makubaliano hayo.