Mej. Jen. Baqeri apongeza harakati za muqawama Palestina kwa ushindi mkubwa
-
Meja Jenerali Mohammad Baqeri
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe kwa mnasaba wa ushindi mkubwa na wa kihistoria wa wapigana jihadi wa Palestina katika makabiliano na utawala vamizi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Katika ujumbe huo Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumamosi ametuma ujumbe akiashiria mapigano na makabiliano ya makundi ya wapigana Jihadi wa Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia Quds Tukufu na kusema: "Vita hivyo vimeendelea kwa muda wa siku 12 na kisha Wazayuni wakachukua hatua ya upande mmoja ya kutangaza usitishwaji vita." Amesema ushindi huo mkubwa wa taifa lililodhulumiwa la Palestina katika jiografia ya Intifadha umeweka wazi ukweli kuwa, uhai wa Wazayuni maghasibu wanaoishi katika nyumba ya kioo uko mikononi mwa Mujahidina wa Palestina na hivyo ni harakati za mapambano ya Kiislamu zitakazoainisha hatima ya medani.
Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema matukio ya hivi sasa katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na mauaji ya kinyama na ya kikatili dhidi ya wanawake, watoto na wanaume wasio na hatia wa Palestina yalipelekea kuibuka oparesheni ya 'Panga la Quds' au Saiful Quds. Amesema oparesheni hiyo inakumbusha namna utawala wa Kizayuni ulivyoshindwa katika vita vya Siku 33, Siku 22, Siku 8 na Siku 51.
Kamanda huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema ushindi huo umeonesha fahari wapigania ukombozi wa Palestina na kudhalilishwa na kushindwa Wazayuni maghasibu na hivyo kutoa bishara ya mustakabali mwema wa ushindi mkubwa kwa Wapalestina.
Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima yatakuwa pamoja na mataifa ya Waislamu wanaodhulumiwa duniani na kwa kumfuata Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, yataendelea kuiunga mkono Palestina na kuimarisha nguvu za Intifadha, kwani hilo ni jambo lilisoloweza kusitishwa. Amesema ajenda ya kudumu ya majeshi ya Iran ni ukombozi wa Quds tukufu na kuwaondoa maghasibu khabithi katika ardhi hiyo.