Safavi: Ushindi wa taifa la Palestina ni matunda ya chuo cha muqawama
Msaidizi na Mshauri Mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, ushindi wa Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 12 vilivyomalizika hivi karibuni, ni matunda ya chuo cha muqawama kilichoimari katika vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu taifa la Iran.
Meja Jenerali Rahim Safavi alisema hayo jana (Jumatatu) na kuongeza kuwa, ushindi wa Wapalestina katika vita vya siku 12 dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni ni matunda ya chuo cha muqawama na cha shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na yote hayo ni matunda ya muqawama wa taifa la Iran katika vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq, dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Meja Jenerali Safavi amegusia pia vielelezo vya nguvu za taifa la Iran vilivyopelekea taifa hili kuukomboa mji wa Khorramshahr kutoka kwa wanajeshi vamizi wa Saddam Hussein na kusisitiza kuwa, ukombozi wa Khorramshahr ulisababishwa na vitu kama mshikamano imara wa kitaifa, umoja na ushirikiano mzuri baina ya jeshi la Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Jeshi la Basiji, Jihadi na Ujenzi na kujitolea jeshi la watu 70 elfu la wananchi katika Basiji na jihadi ya ujenzi nchini Iran.
Mshauri huyo Mkuu wa Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran aidha amesema, matukio mbalimbali, michakato na mikakati tofauti ya Tehran katika kipindi cha takriban miaka 40 iliyopita, ni kuelekea kwenye kuongeza kadiri inavyowezeka nguvu zake za kitaifa. Sasa hivi taifa la Iran ni dola lenye nguvu kubwa kieneo kiasi kwamba Marekani na Wazayuni wanaendelea kushindwa mtawalia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.