Zarif: Iran ni mshirika mwenye kuaminika wa Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe kwa mnasaba wa Siku ya Afrika na kusema: "Iran daima itakuwa mshirika mwenye kuaminika wa marafiki wote Afrika".
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo jana Jumanne katika ujumbe wa Twitter alioutuma kuwapongeza watu wa Afrika kwa mnasaba wa Siku ya Afrika.
Ameongeza kuwa, Iran inasimama pamoja na Afrika na iliweza kupata ilhamu kutokana na ushindi wa Afrika katika kukabiliana na madola ya kibeberu.
Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema huku janga la COVID-19 likieneza uharibifu duniani, kwa mara nyingine Iran imejiunga na wengine katika mapambano dhidi ya 'Apathaidi ya Chanjo'.
Ikumbukwe kuwa Mei 25 miaka 58 iliyopita, hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo. Sikuu hii huadhimishwa kama Siku ya Afrika.
Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 55 wanachama.
Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo.