Araqchi: Bado kuna maudhui muhimu hazijafikiwa makubaliano katika mazungumzo ya JCPOA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamika leo Jumatano na baada ya kumalizika kikao cha kamati ya pamoja ya JCPOA mjini Vienna Austria amesema kuwa, bado kuna maudhui muhimu hazijafikiwa makubaliano. Amesema, maadamu manufaa ya Iran hayajadhaminiwa, mazungumzo ya kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA yataendelea.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Sayyid Abbas Araqchi ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa, hakutaja kwa kina masuala yaliyobakia na muda unaohitajika kufikia makubaliano isipokuwa amesema, bado kuna masuala muhimu yamebakia lakini idadi yake imepungua.
Pamoja na hayo amesema, wajumbe wengi katika maungumzo hayo wana imani kwamba duru hii ya mazungumzo itakuwa ya mwisho na makubaliano kamili yatafikiwa.
Amesema, kila chenye manufaa ya kitaifa kwa Iran lazima kiheshimiwe kwa dhati na matakwa hayo ya Iran lazima yatajwe kwenye maandishi na vipengee vya makubaliano hayo.
Jana Jumanne duru ya tano ya mazungumzo kuhusu kufutwa vikwazo vya Marekani na uwezekano wa kurejea nchi hiyo katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA, ilianza katika kamati ya pamoja ya JCPOA mjini Veinna Austria.
Wakati wa urais wa Donald Trump huko Marekani, rais huyo mwenye chuki za kidini aliitoa Washington katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA licha ya kwamba Marekani ilikuwa mstari wa mbele kuyafikisha kwenye makubaliano kamili mwaka 2015.
Rais wa hivi sasa wa Marekani anadai hakubaliani na uamuzi huo wa rais aliyemtangulia, hata hivyo anaweka vikwazo na masharti mengi, na hairejeshi Marekani katika hali iliyokuwa nayo ndani ya JCPOA baada ya kufikiwa kwake mwaka 2015.