Mwanachuoni wa Kisunni Iran aasa ushiriki mkubwa katika uchaguzi wa rais
Mwanachuoni mmoja wa Kisunni ambaye pia ni Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Iranshar, ulioko katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito wa kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi ujao wa rais hapa nchini.
Mowlavi Abdulsamad Karimzai ametoa mwito huo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kueleza kuwa, ushiriki mkubwa katika uchaguzi utazima hujuma na njama za maadui ambao wameazimia kuwavunja moyo wananchi wa Iran.
Amesema wakazi wa mkoa wa Sistan Baluchestan daima wamekuwa wakizima njama za maadui kwa kushiriki kwa wingi katika chaguzi, na mara hii pia watafuata mkondo huo.
Mwanachuoni huyo wa Kisunni nchini Iran amebainisha kuwa, changamoto zinazolikabili taifa la Iran hazipaswi kufungamanishwa na Mapinduzi ya Kiislamu au Mfumo wa Kiislamu; na kwamba wawakilishi na wasimamizi dhaifu wanapaswa kutimuliwa kupitia uchaguzi, kwani ndio wanaolisababishia matatizo taifa.
Mowlavi Abdulsamad Karimzai ameongeza kuwa, mabadiliko chanya yatapatikana kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi, na kwa kuwachagua viongozi wanaofaa.
Tayari Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetaja majina ya wagombea wa urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Juni.
Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa 6 wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 18 mwezi ujao wa Juni.