Nchi saba zimetangaza azma ya kununua chanjo ya COVID-19 ya Iran
Nchi saba duniani zimetangaza nia ya kununua chanjo ya virusi vya corona ya Iran inalojulikana kwa jina la 'COV-Iran Barakat'
Hayo yamedokezwa na Dkt. Hassan Jalili mkuu wa timu ya utengenezaji chanjo hiyo katika Idara ya Utafiti ya Taasisi ya Utekelezaji wa Maagizo ya Imam Khomeini (MA).
Akizungumza na waandishi habari, Dkt. Jalili amesema uuzaji nje ya nchi chanjo ni jukumu la Wizara ya Afya lakini pamoja na hayo nchi saba zimewasiliana na idara hiyo kwa ajili ya kununua chanjo ya COV-Iran Barekat. Amesema baada ya Iran kukidhi mahitaji yake ya ndani ya nchi, Wizara ya Afya inaweza kutangaza uwezo wa kuuzwa nje chanjo.
Wakati huo huo, Dkt. Jalili amesema tayari wameshazalisha dozi milioni moja za chanjo hiyo ambayo awamu yake ya tatu ya majaribio imekamilika. Amesema dozi hizo zitakabidhiwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kusambazwa nchini. Amesema hivi karibuni hivi wanatarajia kuzalisha dozi milioni 18 za chanjo ya COV-Iran Barekat.
Hivi karibuni kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha dozi milioni 3 za COV-Iran Barekat kilizinduliwa na kwa mujibu wa makadirio wananchi wa Iran wataanza kudungwa chanjo hiyo kati kati ya mwezi Juni.
Iran iko mstari ya mbele kuunda chanjo za COVID-19 ambapo mbali na chanjo ya COV Iran Barakat , chanjo zingine ambazo zimepiga hatua nzuri katika majaribio ni pamoja na Razi Cov Pars, Fakhra na chanjo ya pamoja ya Taasisi ya Chanjo ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran.