Ayatullah Khamenei: Njia ya kufidia mapungufu ni kufanya uchaguzi sahihi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i70890-ayatullah_khamenei_njia_ya_kufidia_mapungufu_ni_kufanya_uchaguzi_sahihi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amehutubia taifa kwa mnasaba wa kukumbuka tukio chungu la kuaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran Imam Ruhullah Khomeini akitilia mkazo udharura wa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa rais na mabaraza miji na vijiji. Amesema kuchagua mtu sahihi na anayefaa ndiyo njia ya kuondoa mapungufu na matatizo yaliyopo.
(last modified 2026-08-01T13:19:30+00:00 )
Jun 04, 2021 06:11 UTC
  • Ayatullah Khamenei: Njia ya kufidia mapungufu ni kufanya uchaguzi sahihi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amehutubia taifa kwa mnasaba wa kukumbuka tukio chungu la kuaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran Imam Ruhullah Khomeini akitilia mkazo udharura wa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa rais na mabaraza miji na vijiji. Amesema kuchagua mtu sahihi na anayefaa ndiyo njia ya kuondoa mapungufu na matatizo yaliyopo.

Ayatullah Ali Khamenei ambaye hotuba yake imerushwa mubashara katika televisheni ya taifa, ameashiria sisitizo la Imam Khomeini la udharura wa kushiriki kwa wingi wananchi katika chaguzi mbalimbali hapa nchini, na kusema kuchagua mtu anayefaa na sahihi ndio suluhisho la mapungufu na matatizo mbalimbali. Ameeleza nukta muhimu zinazohusiana na udharura wa Rais ajaye wa Jamhuri kutekeleza uadilifu wa kijamii, kupambana ipasavyo na bila ya huruma na ufisadi na kuimarisha uzalisha na akasema kuwa: Wananchi wa matabaka yote wanapaswa kushiriki katika uchaguzi na kuwahamasisha wenzao kufanya hivyo.

Vilivile ameashiria kipindi cha awali cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na jinsi mabeberu wa kimataifa walivyokuwa wakitabiri kusambaratika mapinduzi hayo katika kipindi cha miezi miwili, 6 au mwaka mmoja na kusema: Kusimama kidete kwa Imam Khomeini, misimamo yake imara, ushindi mkubwa wa taifa katika vita na masuala mengineyo, yote hayo yalibatilisha utabiri wa mabeberu. Ameongeza kuwa baada ya kuaga dunia hayati Imam Khomeini maadui walikariri matarajio yao hayo ya kusambaratika Jamhuri ya Kiislamu. 

Imam Ruhullah Khomeini

Ayatullah Khamenei ameashiria pia maendeleo na ustawi endelevu unaoshuhudiwa hapa nchini na kusema: Siri ya kubakia hai mfumo wa Imam Khomeini ni kuendelea kushikamana ka mambo mawili yaani Jamhuri (yani wananchi) na Uislamu. 

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, miongoni mwa kazi kubwa zilizofanywa na Imam Khomeini ni kubuni fikra ya Jamhuri ya Kiislamu na kuingiza fikra hiyo katika nadharia za kisiasa za kimataifa na hatimaye kutekeleza nadharia hiyo kivitendo.

Amefafanua zaidi kwa kusema kuwa maneno mawili ya "Jamhuri"  na "Kiislamu" kwa maana ya utawala wa Uislamu na wananchi, ndio ufunguo wa matatizo yote na kuongeza kuwa: Wakati wote wananchi wanaposhirikishwa na vigezo vya Uislamu vikazingatiwa, tulipiga hatua za maendeleo; na pale majawapo kati ya mawili hayo halikuzingatiwa na kuchungwa, tulikwama na kutuama.